Jumanne , 21st Mei , 2024

Mkoa wa Tanga umetajwa kuwa unashika nafasi ya pili ya utumiaji wa dawa za kulevya Kitaifa, hali ambayo imewasukuma wadau wanaojihusisha na mapambano dhidi ya dawa hizo kukutana ili kufanya tathimini na hali ya utumiaji wa dawa za kulevya kujadili namna nzuri ya kuwafikia waathirika.

Dawa za Kulevya

Wakizungumza kwenye kikao hicho pamoja na mambo mengine wadau hao wameiomba jamii kuwasaidia waraibu badala ya kuishia kuwaadhibu ikiwa ni njia bora ya kuwabadilisha na kurudi kwenye hali zao za awali. 

Mkuu wa kitengo cha Methadone katika hospitali ya rufaa ya Mkoa Tanga, Bombo Dkt. Wallace Karata ameishukuru serikali kwa kuondoka katika mpango wa kuwakamata na kuwaweka rumande watumiaji wa dawa hizo na badala yake wanawataka waraibu waliokuwa tayari kupata huduma kujitokeza kwenye vituo vya afya ili wapate huduma ya matibabu kulingana na hali zao. 

"Dawa za kulevya ni tatizo la dunia nzima lakini Tanzania na sisi tukiwa kama sehemu ya dunia na sisi limetukuta na tumepata athari kubwa na bahati mbaya Mkoa wetu wa Tanga unaongoza kwa matumizi lakinj tuishukuri serikali yetu kwamba sasa imeondoka katika mpango wa kamata kamata na kuwaweka jela lakini wameona waraibu walio tayari kutibiwa wajitokeze, "alisisitiza Dkt Karata. 

Wakizungumza kwenye kikao hicho waraibu waliopata nafuu wamesema huduma ya Methadone inayotolewa imewasaidia kubadilika na kuongeza imani kwa jamii ambayo hapo awali ilikuwa ikiwanyanyapaa kutokana na tabia zao. 

Kwa mujibu wa kituo cha kutolea huduma ya Methadone (MAT)  jumla ya waraibu 1094 wamejiandikisha kwenye huduma ya Methadone katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Tanga Bombo na kwamba bado jitihada mbalimnali zinafanywa ili kuhakikisha waraibu wote wanapata huduma hiyo kwajili ya utengamao. 

Kikao cha kutathimini na kujadili utendaji wa Programu ya Utekelezaji wa Mradi wa Afya Hatua iliyopo chini ya Shirika la THPS na kufadhiliwa na Pepfar kupitia CDC kimeketi Jijini Tanga na kuhusisha wadau mbalimbali Mkoani Tanga wa mapambano dhidi ya dawa za kulevya kutokana na Mkoa huo kushika nafasi ya pili kwa watumiaji kitaifa.