Alhamisi , 13th Dec , 2018

Matukio ya ukatili wa kijinsia mkoani Geita bado ni tishio kubwa na yanazidi kuongozeka baada ya wanawake 12 kuuawa kinyama ikiwa ni pamoja na kunyofolewa baadhi ya viungo vya miili yao yakiwemo matiti na sehemu za siri.

Mbali na wanawake hao, pia  watoto wawili wameuawa kikatili mkoani humo, wanafunzi 160 wakikatishwa masomo yao kwa kubeba mimba wilayani  Nyang’hwale mkoani humo ambapo matukio hayo yote yametokea katika kipindi cha mwaka 2017/18.

Chanzo cha matukio hayo kimetajwa kuwa ni imani za kishirikina na ndoa za utotoni na kulilazimu Shirika la Kimataifa la Plan kwa kushirikiana na Serikali mkoani Geita kuadhimisha kilele cha siku 16 za kupinga ukatili wa kijinsia katika Wilaya ya Nyang’hwale.

Tukio la wanawake watatu waliouawa huko Nyang’hwale kwa kunyongwa shingo wakitoka shamba bado hazijafutika masikioni mwa wanawake, huku watoto wa kike wakidai kuwa umbali mrefu wa kwenda shule ndicho chanzo cha vishawishi wakiwa njiani.

Maadhimisho ya siku 16 ya Kupinga ukatili wa kijinsia hufanyika kuanzia Novemba 25 – Disemba 10 ya kila mwaka na Mwaka huu yamefanyika yakiambatana na Kauli Mbiu “Funguka Usalama wako Wajibu Wangu”