Jumanne , 7th Jun , 2016

Baadhi ya wakazi wa Jiji la Mwanza wameiomba serikali kuimairisha ulinzi kwenye mapango yalipo Jijini humo ili yasigeuzwe kuwa maficho ya wahalifu kama ilivyobainika hivi karibuni.

Polisi Jijini Mwanza wakiwa katika harakati za kupambana na Majambazi katika mapango ya Utemini.

Wakazi hao wametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Wilaya ya Nyamagana katika mapango ya Utemini, ikiwa ni siku moja tu baada ya watu watatu wanaodhaniwa kuwa ni majambazi kuuawa katika mapango hayo walipopambana na Polisi.

Akizungumza katika ziara hiyo Mwenyekiti wa Mtaa wa Utemini, Michael Kiula, amewataka wakazi wa maeneo hayo kutoa taarifa haraka kwa mamlaka husika pindi wanapowaona watu wanaowatilia shaka katika mapango hayo.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Nyamagana, Baraka Konisaga, ametumia fursa hiyo kuwatoa hofu wakazi wa maeneo hayo na kusema kuwa serikali haitalala na itahakikisha inapambana na wahalifu wote watakaojitokeza na waliopo katika eneo hilo.