Jumanne , 17th Mei , 2022

Katibu Mkuu wa Katiba na Sheria, Bi. Mary Makondo amewataka wahariri  na waandishi wa habari kupata mafunzo maalumu kuhusu kuripoti taarifa zinazohusiana na vitendo vya ukatili wa kijinsia katika jamii zetu.

Amesema hayo wakati wa  ufunguzi wa mafunzo ya siku mbili ya namna ya utoaji taarifa za ukatili wa kijinsia kwa Wahariri na Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini , mafunzo yaliyofanyika jijini Arusha.

Bi. Makondo amesema lengo la mafunzo hayo ni kujengeana uwezo, kujifunza, kubadilishana uzoefu, mbinu na kujadiliana kuhusu nafasi ya Waandishi wa Habari na Wahariri katika kutokomeza ukatili wa kijinsia katika jamii zetu.

Bi. Makondo amesema kumekuwa na ongezeko la matukio ya ukatili na unyanyasaji wa kijinsia na uhalifu kama vile, ubakaji, ndoa za utotoni, ukeketaji, ukatili wa majumbani, wajane kupokwa mali za wenza wao na mauaji. 

"Katika kukabiliana na ukatili wa kijinsia, Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuwashirikisha wadau wake katika mapambano hayo. Miongoni mwa hatua hizo ni pamoja na kuimarisha mifumo ya kisheria na utoaji haki, huduma za afya, elimu, kuanzisha vituo vya huduma kwa manusura wa ukatili na kuwafikisha kwenye vyombo vya dola, ikiwemo mahakamani wote wanaotuhumiwa na makosa ya ukatili. " amesema Bi. Makondo. 

Aidha, Serikali imewezesha kutungwa kwa sheria ya Msaada wa kisheria kwa lengo la kumeimarisha upatikanaji haki kwa watu wasio na uwezo wa kumudu gharama za mawakili. Kwa sasa Wananchi wana uwezo wa kutafuta na kupata afua za kisheria kwa kutumia njia mbadala za utatuzi wa migogoro nje ya Mahakama. Haya yote ni juhudi za Serikali kupitia Wizara ya Katiba na Sheria na kwa kushirikiana na wadau mbalimbali wakiwemo Wahariri na Waandishi wa habari.

Bi. Makondo ametoa rai kwa Wanahabari kuzingatia maadili ya uandishi na kulinda waathirika wa unyanyasaji wa kijinsia wakati wa utoaji taarifa ili kuepuka athari zaidi kwa wahanga wa matukio haya.