Alhamisi , 9th Jun , 2016

Wanafunzi 480 waliofukuzwa katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Joseph kwa madai ya kutokuwa na sifa za kudahiliwa kwenye vyuo vikuu nchini wamefungua kesi Mahakamani.

Akithibitisha kufunguliwa kwa kesi hiyo, Wakili wa wanafunzi hao, Emanuel Muga, ameiambia East Africa Radio kuwa kesi hiyo imefunguliwa katika Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam chini ya Jaji Eliezer Feleshi na kwamba katika madai hayo, wanafunzi hao pia wametaka masomo kusimamishwa katika chuo hicho mpaka mahakama itakaposikiliza kesi yao ya msingi.

Wakili Muga amesema kesi hiyo namba 311 ya mwaka 2016 inatarajiwa kuanza kutajwa kesho ambapo wanafunzi 316 kati ya 480 ya waliofukuzwa ndio wamefungua kesi wakidai haki ya kisheria kuingilia kati maamuzi yaliyofanywa na serikali

Kwa upande mwingine Wakili Muga amewataka wanafunzi waliofukuzwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma kudai haki yao Mahakamani na kuacha kulalamika kwani Mahakama pekee ndio inatoa haki kwa mtu aliyeonewa