Ijumaa , 11th Aug , 2023

Wanafunzi na walimu wa shule ya msingi Uhuru, Kata ya Mwakibete Jijini Mbeya wamemuomba Mbunge wa jimbo hilo na Spika wa Bunge Dkt Tulia Ackson, awasaidie kuboresha miundombinu ya madarasa, vyoo pamoja na madawati kwani iliyopo kwa sasa haitoshelezi na mingine ni chakavu na si rafiki.

moja ya tundu la choo kwenye shule hiyo

Mwalimu Mkuu wa shule hiyo Agnes Mwila amesema shule yake ina idadi ya wanafunzi 1880 na mahitaji ni matundu 84, na yaliyopo kwa sasa ni matundu 18 jambo ambalo haliendani na uwiano wa idadi ya wanafunzi na kuongeza kwamba pia wana upungufu wa madawati 200 na sakafu ya madarasa imebomoka si rafiki kwa watoto.

"Tunauhitaji wa madawati 200 na kwa upande wa vyoo matundu yapo machache tunayo 18 na watoto wapo 1880 hivyo hayatoshelezi kwani mahitaji ni 84 lakini pia madarasa yamechimbika yana mashimo sababu ni muda mrefu kuna mashimo hata ukipita unaweza kujikwaa," amesema Mwalimu Agnes Mwila.

Baada ya kilio hicho Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson amesema asingependa kuona watoto wanakaa chini hivyo amekubali kutoa msaada wa madawati 200, kufanya ukarabati wa madarasa na kufanya mpango wa ujenzi wa vyoo vya shule hiyo.