Jumanne , 28th Apr , 2015

Msafara wa Makamu wa Rais, Dk Mohammed Gharib Bilal, mkoani , umelazimika kuchepushwa barabara kufuatia mgomo wa wanafunzi wa chuo cha ualimu (Elimu maalum) Patandi, uliosababisha kufungwa kwa njia.

Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mohammed Gharib Bilal.

Watu walioshuhudia wamesema polisi wamelazimika kuwarushia wanafunzi hao mabomu ya machozi kwa lengo la kuwatawanya.

Wanafunzi wamegoma mapema jana asubuhi na kufunga barabara kuu ya kutoka Moshi kwenda mjini Arusha kwa kutumia mawe kwa muda wa takriban saa moja kuanzia saa 4 hadi 5 asubuhi kabla ya msafara wa Makamu wa Rais kupita eneo hilo.

Makamu wa Rais na msafara wake wakitokea Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), alikuwa apite hapo kuelekea Taasisi ya Nelson Mandela ya Sayansi na Teknolojia Afrika (NM-AIST).

Katika taasisi hiyo ambayo ni mkuu wa chuo, alialikwa kuwa mgeni rasmi, kufungua mkutano wa kimataifa wa ‘Kujifunza pamoja kwa ajili ya kuleta mabadiliko: Kuendeleza elimu bora ya juu kwa wote.’

Wakizungumza chuoni hapa leo, wanafunzi hao wamesema lengo la mgomo wao ni kushinikiza mkuu wa chuo aondolewe.

Wanadai kuwa mkuu wa chuo hicho Zaina Mbelwa, anawapa adhabu za shule za msingi kama kuwapigisha magoti mbele ya bendera ya taifa, kuwapiga makofi na kuwafanyisha usafi wakati wanatoa Sh. 30,000 za kufanyiwa usafi.

Mkuu wa polisi wa kituo cha Usa River, Msolo Msolo, amesema wamelazimika kutumia mabomu ya machozi kuwatawanya wanafunzi na kutuliza hali ya hewa.

Amesema kutokana na vurugu hizo wamelazimika kupitisha msafara wa Makamu wa Rais katika barabara ya vumbi na kuacha ya lami.

Akizungumzia tukio hilo, Mkuu wa Chuo Mbelwa, amesema wanafunzi hao wamefanya hayo kwa sababu ya kuwabana ili wafuate sheria na kanuni za chuo.

Amesema baadhi ya wanafunzi wanavuta bangi na kutumia dawa za kulevya na hivyo kuvunja sheria na kanuni za chuo.

Pia amesema baadhi yao wanatembea na walimu kimapenzi badala ya kufuata masomo na pale wanapolazimika kuwakagua wanagoma.

Kuhusu fedha za usafi, amesema wanalipa Sh. 15,000 na sio Sh. 30,000 kama wanavyodai.

Amekiri kuwaadhibu wanafunzi wanaokiuka sheria na kanuni tena wengine hawahudhurii masomo na badala yake wanasikiliza redio.

Kwa upande wa chakula amesema kuna tatizo ambalo sio lake, ni la mzabuni ambaye amegoma kuleta mboga akidai hajalipwa Sh. Milioni 220 za mwezi Machi.

Akizungumzia kuhusu uongozi wa wanafunzi, amesema wanafunzi hao hawana uongozi na ndio maana tatizo hilo limejitokeza.

Katika mazungumzo na polisi jana, wamemshauri kuitisha uchaguzi wa viongozi wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo mapema.