Jumatano , 15th Apr , 2015

Watu nane waliokufa baada ya kupigwa na radi jana kufuatia mvua iliyonyesha kwa takriban masaa matatu mkoani Kigoma wameagwa leo katika viwanja vya shule ya msingi Kibirizi mkoani humo.

Vilio na simanzi vimetawala wakati mkuu wa mkoa wa Kigoma Luten Kanal mstaafu Issa Machibya akiwaongoza mamia ya wakazi wa manispaa ya kigoma ujiji kuaga miili ya watu nane waliokufa baada ya kupigwa na radi jana kufuatia mvua iliyonyesha kwa takriban masaa matatu.

Miongoni mwa watu hao ni wanafunzi sita wa darasa la kwanza katika shule ya msingi Kibirizi mjini kigoma.

Majonzi yalitawala shughuli hiyo hasa baada ya miili hiyo kupokelewa katika viwanja vya shule ya msingi kibirizi kabla ya ndugu kukabidhiwa tayari kwa maziko huku mwili wa mwalim Elieza Mbwambo ukisafirishwa kwenda Moshi kwa maziko .

Akitoa salam za rambirambi mkuu wa mkoa wa Kigoma Luten Kanal mstaafu Issa Machibya amewataka wafiwa na wananchi kuchukulia tatizo hilo kama ni tukio la ajali ya kawaida na kwamba msiba huo ni mzito.

Kwa upande wao viongozi wa dini Shekh Moshi Guoguo kutoka BAKWATA na mchungaji Emmanuel Mtoi wa kanisa la KKKT wakitoa mawaidha katika msiba huo, wamewataka waumini wa dini mbalimbali kujiandaa kwa kuwa kila mwanadamu ataonja mauti kwa wakati wake na kwamba imani za kishirikina zisihusishwe katika msiba huo.