Serikali imetengua uteuzi wa wakurugenzi 6 wa halmashauri, na hivyo kuwasimamisha kazi wengine watano ili kupisha uchunguzi kufanyika.
Kutenguliwa uteuzi huo na wengine kuwekwa pembeni kupisha uchunguzi ni kufuatia kubainika kuchangia kuvurugika kwa uchaguzi wa Serikali za Mitaa uliofanyika Jumapili wiki iliyopita ya Desemba 14 nchini Tanzania.
Uamuzi huo unatokana na Ripoti iliyouibua kasoro mbalimbali katika uchaguzi huo ambapo Waziri wa nchi ofisi ya waziri mkuu,Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Bi Hawa Ghasia amesema kuwa uamuzi wa kutenguliwa nyadhifa walizo kuwa nazo wakurugenzi hao umeridhiwa na Rais Kikwete.
Aidha ameongza kwa kuweka bayana halmashauri ambazo wakurugenzi hao waliotenguliwa kuwa ni kutoka Mkuranga, Serengeti, Bunda na Kaliuwa, Huku wakurugenzi walio simamishwa kazi ni kutoka, Mbulu, Ulanga, Kwimba, Hanang', Pamoja na manispaa ya Sumbawanga.
Waziri Ghasia amesema kuwa Wakurugenzi wengine watatu wapewa onyo kali, ambao ni wa Rombo, Busege na Muheza na wengine watatu wakipewa onyo la kawaida, wakurugenzi hao ni wa Manispaa Ilala, Hai na Mvomero.
Hatua hiyo imekuja Ikiwa ni siku Tatu sasa tangu Waziri wa TAMISEMI, Hawa Ghasia kuzungumza na vyombo vya habari juu ya hali ilivyokuwa katika uchaguzi wa serikali za Mitaa na kuwa na dosari kadhaa huku ofisi yake ikiwa inashutumiwa kwa kutokuwa thabiti katika hilo na yeye mwenyewe kusema kuwa endapo kama ofisi yake itabainika ilifanya uzembe wowote katika uchaguzi huo atajiuzulu lakini kama wapo watendaji waliofanya uzembe hadi kutokea kwa dosari watawajibishwa na wengine kufukuzwa.