Profesa Ibrahim Lipumba
Kauli hiyo ameitoa hii leo Septemba 22, 2020, kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya jumba la maendeleo wilaya ya Kibondo, na kuongeza kuwa ubovu wa miundombinu ndiyo chanzo cha wananchi kuwa na hali ngumu.
"Tujenge miundombinu, barabara za kwenda vijijini zinapunguza gharama za usafirishaji wa mazao kutoka vijijini, Oktoba 28 mkinichagua mimi kipaumbele changu katika ujenzi wa miundombinu itakuwa barabara hii ya Nyakanazi mpaka Kasulu, na maji ya uhakika yaweze kupatikana Kibondo", amesema Profesa Lipumba.
Aidha Profesa Lipumba ameongeza kuwa,"Watani zangu waha wanajulikana nchi nzima ni wachapakazi wa kweli na wakijengewa mazingira mazuri wataboresha kilimo chao, bila kilimo kilicho bora huwezi ukawa na mapinduzi ya viwanda".
Awali akizungumzia suala la maji Profesa Lipumba amesema , wananchi wa Kibondo wamekuwa wakikabiliwa na tatizo la maji pamoja na kubambikiwa madeni na kuahidi kuwa endapo chama chake kitapata ridhaa kitahakikisha wanakuwa na maji yakutosha.