Wafungwa zaidi ya 6000 waliofungwa katika magereza yaliyopo kwenye mikoa Sita nchini watapatiwa mafunzo ya stadi za kazi ili watakaporejea uraiani baada ya kumaliza kifungo waweze kujikita katika kazi ya ufundi ambayo itawawezesha kujipatia fedha za kujikimu na kuachana na vitendo viovu katika kijamii.
Zoezi hilo la kuwapatia stadi za kazi wafungwa linaratibiwa na shirika la kujali utu wa binadamu linalojulikana kwa jina la ''Dorcas Aid'' ambapo wataanza kazi hiyo kwa awamu kwa wafungwa waliobakisha kipindi kifupi cha kifungo kuanzia miezi sita hadi mwaka mmoja ili waweze kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza wilayani Handeni kuhusu mchakato wa kusaidia watu wasiojiweza nchini,afisa mipango wa shirika la ''Dorcas Aid'' nchini bwana shahada nikuli amewaeleza viongozi wa serikali wilayani humo kuwa mkakati huo utaanza mapema mwakani kwa mkoa wa Kilimanjaro kisha kwenda katika mikoa mingine ikiwemo Tanga, Arusha na Manyara.
Awali mwenyekiti wa serikali ya mtaa wa kwa Masaka iliyopo kata ya kwa Magome wilayani Handeni Bwana Saleh Zonga ameliomba shirika hilo kwa kusaidiana na serikali kuwajengea miundombinu ikiwemo ukarabati wa barabara kwa sababu changamoto hiyo imekuwa kikwazo katika zoezi la kujikwamua na umasikini.