Jumatano , 7th Sep , 2016

Bei ya jumla na rejareja ya nyanya imeshuka katika masoko kadhaa jijini Dar es Salaam, kutokana na ongezeko la ghafla la mavuno ya zao hilo ambalo haliendani na mahitaji halisi ya bidhaa hiyo kutoka kwa walaji.

Makasha ya nyanya katika moja ya soko Jijini Dar es Salaam

EATV imetembelea masoko hayo ambapo katika soko la Temeke Stereo, kasha moja la nyanya hivi sasa linauzwa kwa kati ya shilingi elfu nane na shilingi elfu kumi na mbili, kutoka bei ya awali ambapo kasha hilo lilikuwa linauzwa kwa kati ya shilingi elfu 35 na shilingi elfu 60.

Kufuatia hali hiyo, baadhi ya wauzaji wameiomba serikali kuwasaidia utaalamu pamoja na msingi wa uanzishaji wa viwanda vya kusindika nyanya ili kuepuka hasara wanayoipata hivi sasa na kwamba hatua hiyo itakuwa moja ya utekelezaji wa mpango wa serikali wa uanzishwaji wa viwanda nchini.