Alhamisi , 29th Jun , 2017

Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini IGP, Simon Sirro, ameyataka makundi ya vijana Wilayani Mkuranga, Rufiji na Kibiti Mkoani Pwani kuhakikisha wanaweka vikundi vya ulinzi katika maeneo yao ili kukabiliana na wauaji kwani wanaotekeleza mauaji si wazee.

IGP Sirro ametoa rai hiyo alipokwenda kuwapa pole wananchi wa Kijiji cha Mangwi Kata ya Mchukwi Wilaya ya Kibiti kulipotokea mauaji ya viongozi wawili wa vijiji akiwemo Mwenyekiti wa Kijiji, Afisa Mtendaji wa Kijiji na Mwenyekiti wa Kitongoji cha Londo ambaye alijeruhiwa kwa risasi na kisha kumtoboa macho ambapo ametoa ubani.

IGP amewaambia wananchi kuwa, hakuna haja ya kuilaumu serikali kwa vile maeneo yako mbali na ndio maana wauaji wanatekeleza azma yao kiurahisi kutokana na jiografia ya mkoa huo lakini amesema, ushirikiano wa wananchi na Jeshi la Polisi ni muhimu hata kama doria itafanyika.