Jumapili , 8th Oct , 2023

Jumla ya Waisraeli 300 wameuawa na wengine takribani 2000 wakijeruhiwa huku wengine 100 wakiwemo wanajeshi wakitekwa nyara, kufuatia mashambulio dhidi yake na Palestina hii ni kwa mujibu wa Ubalozi wa Israel nchini Uturuki ukinukuu Wizara ya Afya ya Israel

Mnara wa Palestina ukifuka moshi baada ya kushambuliwa na ndege za kivita za Israel

Aidha taarifa zimeeleza pia jumla ya Wapalestina 313 wameuawa na karibu 2,000 kujeruhiwa huko Gaza kufuatia mashambulizi ya anga ya kulipiza kisasi kutoka Israel tangu jana Jumamosi.

Kwa upande wake Rais wa Marekani Joe Biden amesema kwamba serikali ya Marekani iko bega kwa bega na Israel na kwamba haitoacha kutoa msaada wake wa kiusalama kwa taifa kwani uungaji wake mkono pamoja na serikali yake ni thabiti na hauwezi kutetereka ili kuhakikisha raia wanabaki salama, huku akisisitiza kwamba huu si wakati kwa vyama vinavyoichukia Israel kutumia mashambulizi kati yake na Palestina kujinufaisha.

Umoja wa Afrika AU, umeelezea kusikitishwa na vita hiyo iliyoibuka kati ya Israeli na Palestina ambapo imetoa wito kwa pande zote mbili kukomesha mara moja uhasama wa kijeshi na kurudi kwenye meza ya mazungumzo bila masharti na kutekeleza mpango wa kuunda nchi mbili.

Mwenyekiti wa AU Moussa Faki Mahamat amesema mzozo huo utakuwa na athari mbaya kwa maisha watu ambapo amesema sababu ya vita hiyo ni kukataliwa kwa haki za kimsingi za watu wa Palestina, hususani ile ya kuwa na serikali huru.