Jumapili , 20th Mar , 2016

Taasisi ya Uendelezaji Miundombinu ya UTT Project and Infrastructure Development UTT-PID, imeelezea kusikitishwa na mtu anayeeneza uvumi na kuchafua utendaji wa shirika hilo ili ionekane kama kuna ubadhilifu wa pesa na matumizi mabaya ya madaraka.

Afisa Mtendaji Mkuu wa UTT-PID Bw. Gration Kamugisha (kulia) akizungumza na wanahabari ambao hawapo kwenye picha.

Uchafuzi huo umekuwa ukifanywa licha ya kuwa moja ya taasisi chache za serikali zinazofanya vizuri katika kuokoa fedha za umma kwa kutafuta vyanzo vya mapato na kutekeleza miradi ambayo pengine isingetekelezeka kutokana na ukosefu wa pesa.

Afisa Mtendaji Mkuu wa UTT-PID Bw. Gration Kamugisha amesema hayo katika mkutano wake na wanahabari jijini Dar es Salaam na kutaja baadhi ya vitendo vinavyofanywa vya kuchafua rekodi nzuri ya utendaji wa taasisi hiyo kuwa ni barua zinazoandikwa na mtu ambaye hataki jina lake lijulikane, akidai kuwa taasisi hiyo imekuwa ikiendeshwa kindugu kutokana na watumishi wake wengi kuwa wa kabila moja na kiongozi mmoja wa juu wa taasizi hiyo.

“Kumekuwa na mtu anayeandika barua kwenda taasisi mbali mbali za umma akiwa na nia ya kuchafua sifa na utendaji wa UTT-PID, mtu huyo anafahamu fika kwamba sehemu nyingi duniani barua kama hizo huwa hazifanyiwi kazi lakini kwa lengo la kuchafuana kwa makusudi amekuwa akiandika barua hizo pasipo kutaka ajulikane,” amesema Dkt Kamugisha.

Amesema tatizo hilo limeanza Juni mwaka jana kiasi cha kulazimu bodi ya taasisi hiyo kuitisha mkutano wa wafanyakazi kwa lengo la kupata maoni ya wao ili kuona kama tuhuma zinazotolewa zina ukweli wowote lakini hakuna mfanyakazi hata mmoja aliyeunga mkono madai yanayotolewa kwenye barua hizo zisizokuwa na anuani.

“Baada ya mfululizo wa hizo barua za tuhuma, tuliona kuna haja ya kupata maoni ya watumishi wetu kwani kuna kila dalili mlalamikaji anaweza kuwa mtumishi wa UTT-PID kutokana na ukweli kwamba mtu huyo amekuwa akichukua baadhi ya mambo na mipango inayotekelezwa na taasisi hiyo na kuigeuza kutia uwongo kwa lengo la kuchafuana, lakini cha kustaajabisha ni kwamba wafanyakazi wote walielezea kuridhishwa na utendaji wa viongozi wao,” amesema Dkt Kamugisha na kufafanua,
“Baada ya tuhuma hizo hewa tukaona ni vyema Watanzania wakafahamu kinachoendelea ndani ya taasisi yetu kwani baada ya kuona hoja zake zinapuuzwa kila alikozipeleka, huyo mtu sasa amegeukia vyombo vya habari na kuanza kutumia magazeti kuendelea na kampeni yake hiyo chafu ambayo kimsingi inarudisha nyuma utendaji wetu kwani tunajikuta tunaanza kutumia muda mwingi kujibu na kushughulikia tuhuma zake wakati tungetumia muda huo kutekeleza miradi ya maendeleo,”

Aidha, akitaja majukumu ya UTT-PID, Dkt Kamugisha amesema serikali inaweza kuokoa kiasi kikubwa cha pesa wakati huohuo ikitumia muda mfupi katika kutatua kero za wananchi iwapo itaitumia taasisi ya uendelezaji miundombinu ya UTT Project and Infrastructure Development kama mfadhili wa kifedha na mtekelezaji wa miradi husika ya maendeleo.

Dkt. Kamugisha amesema hayo hii leo na kutaja miradi ya kiuchumi ambayo taasisi yake inaweza kuokoa pesa za serikali iwapo itapewa kuitekeleza kuwa ni ujenzi wa masoko, maeneo ya kutolea huduma kama hospitali na upimaji ardhi.