Jumapili , 7th Feb , 2016

Waokoaji ambao wanaendelea na zoezi la kuokoa watu waliofukiwa na vifusi baada ya kutokea Tetemeko la ardhi nchini Taiwan na kuangusha ghorofa, wamesema zoezi hilo halitafanikiwa kuokoa watu wote au kutoa miili yao zaidi ya103 iliyokwama.

Waokoaji hao wamekiri udhaifu huo kutokana na ukubwa wa jengo la ghorofa 17 ambalo limeanguka, kusini mwa mji wa Tainan na kufunika watu hao.

Vifaa mbali mbali vya uokoaji vinatumika katika zoezi hilo, pamoja na mbwa wanaonusa harufu kutambua kama kuna uhai wa mtu mahali hapo.

Zaidi ya watu 240 wameshaokolewa kutoka kwenye jengo hilo, na mapka sasa takriban watu 23 wamethibitishwa kufariki.

Taarifa zinasema kwamba sauti za watu wakiomba msaada zinasikika kutoka kwenye jengo hilo, na watu 475 wameripotiwa kujeruhiwa kutokana na tetemeko hilo.

Tetemeko hilo lenye ukubwa wa magnitude 6.4, limeibua maswali mengi ikiwemo ubora wa vifaa vilivyotumika katika ujenzi wa ghorofa hilo, lililojengwa miaka ya 90.