Alhamisi , 19th Mar , 2015

Kaimu Kamishna wa Uhamiaji nchini Tanzania Peniael Mgonja amewataka maafisa wa uhamiaji kutoka maeneo mbalimbali ya nchi kuzingatia suala la utunzaji wa mazingira katika maeneo yao ya kazi.

Hii ni picha ya moja ya mazingira yaliyotunzwa vizuri.

Bw. Mgonja ametoa ushauri huo leo jijini Dar es Salaam wakati alipokutana na maofisa hao kwa lengo la kuwaeleza namna idara ya uhamiaji nchini itakavyotekeleza sera ya uhifadhi bora wa mazingira.

Amesema idara ya uhamiaji sasa ina wajibu wa kuhakikisha kwamba utunzaji wa mazingira katika maeneo ya kazi ni jukumu ambalo linahitajika kusimamiwa ipasavyo badala ya kuliona kama ni jukumu la taasisi moja pekee ya serikali.

Aidha amewataka wakuu hao wa idara na taasisi mbalimbali zinazosimamia masuala ya uhamiaji nchini kutoa elimu hiyo kwa wananchi wanaowazunguka kwa lengo la kuelewa umuhimu wa kutunza mazingira.

Amesema utunzaji wa mazingira umekuwa na faida nyingi ikiwemo kuepukana na magonjwa ya milipuko, kupata hewa safi inayotokana na miti kutokukatwa hovyo jambo ambalo amesema ni lazima lisimamiwe kikamilifu.