Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli.
Akiongea leo Jijini Dar es Salaam, katika utoaji wa tuzo za rais kwa wazalishaji bora viwandani kwa mwaka 2015, Rais wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema kuwa bidhaa kutoka nje zitawekewa umakini ili zisiharibu soko la bidhaa zinazozalishwa na viwanda vya ndani.
Rais Dkt. John Magufuli amesema kuwa kwa kauli yake hiyo sio kwamba anawachukia wawekezaji kutoka nje lakini ameona ni vyema kuweka uzalendo mbele ili kukuza uchumi wa nchini kupitia wawekezaji wa ndani lakini na pia kuongeza ajira hususani kwa vijana kupitia viwanda hivyo.
Dkt. Magufuli ameongeza kuwa kuna viwanda vingi vilikufa nchini kutokana na wawekezaji wasiokuwa na uwezo ambao wengi wao walipelekea kushindwa kufanya uzalishaji na kusababisha viwanda hivyo kufa.
Pamoja na mambo mengine Dkt. Magufuli amemtaka Waziri wa Viwanda na Biashara kutengeneza sera ambayo itawafanya wawekezaji na wafanyabiashara kutoka nje ya nchi kutozwa kodi kubwa ili kuwalinda wazalishaji wa ndani.