Jumatano , 4th Mar , 2020

Upande wa mashtaka katika kesi ya uhujumu uchumi, inayomkabili Afisa wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tito Magoti na mwenzake Theodory Giyan, umeshindwa kusema upelelezi wa kesi hiyo ulipofikia kwa madai ya kuwa jalada la upelelezi wa kesi hiyo bado liko Polisi.

Tito Magoti na mwenzake Theodory Giyan, wakiwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.

Hayo yamebainishwa leo Machi 4, 2020, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu Jijini Dar es Salam, na Wakili wa Serikali Wankyo Simon na kusema kuwa kwa sasa hawajui kinachoendelea kwenye upelelezi wa kesi hiyo, kwani jalada bado lipo Polisi na litakapokamilika watalipeleka Ofisi ya Mwendesha Mashtaka.

Baada ya maelezo hayo Hakimu Mkazi Mwandamizi wa Mahakama hiyo, Janeth Mtega, aliahirisha kesi hiyo hadi Machi 18, 2020 itakapotajwa tena.

Magoti na mwezake Theodory wanakabiliwa na mashtaka matatu, ikiwemo utakatishaji wa fedha kiasi cha Shilingi milioni 17, matukio ambayo wanadaiwa kuyatenda Jijini Dar es Salaam na maeneo mbalimbali ya nchi.