Alhamisi , 11th Feb , 2016

Ofisi ya waziri mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania TAMISEMI imesema itaajiri madaktari wapatao 10,780 ili kukabiliana na uchache wa madaktari nchini.

Ofisi ya waziri mkuu Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa nchini Tanzania TAMISEMI imesema itaajiri Madaktari wapatao 10,780 ili kukabiliana na uchache wa madaktari nchini hali inayochangia kwa kiasi kukubwa kuongezeka kwa vifo vitokananavyo na magonjwa yanayoweza kuzuilika.

Hayo yameelezwa na Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Selemani Jaffo wakati wa mkutano wa mwaka wa kujadili masuala ya afya uliowakutanisha watunga sera wa sekta mabalimbali za afya pamoja na wadau wa afya nchini.

Kwa mujibu wa Shirika la Mkapa Foundation, asilimia 74 ya madaktari nchini Tanzania wanapatikana katika maeneo ya mijini, kwa sasa daktari mmoja anahudumia wagonjwa 78,880 maeneo ya vijijini huku mijini Daktari mmoja anahudumia wagonjwa 9,095, mapendekezo ya shirika la afya duniani uwiano ni daktari mmoja kuhudumia wagonjwa 10,000.

Kufuatia hali hiyo Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Selemani Jaffo amesema kuwa ofisi yake itahakikisha kuwa wananchi wanafikiwa na huduma za afya zikiwemo dawa katika zahanati na vituo vyote vya afya nchini kwa kuwa na Zahanati katika kila kata pamoja na kuajiri madaktari wapya.

Sekta ya afya nchini Tanzania inahitaji watumishi wapya 145,454 ili kutoa huduma bora za afya ,hadi kufikia mwaka 2014 idadi ya watumishi wa afya nchini walikuwa 70244 na kuwa na upungufu wa watumishi 75,211 sawa na asilimia 52.

Akizungumzia hali hiyo Waziri wa Afya Maendeleo ya Jamii Wazee na Watoto nchini Tanzania, Mhe.Ummy Mwalimu amesema Sekta ya afya inakabiliwa na changamoto nyingi ikiwa ni pamoja na upungufu wa watumishi wa afya kwa asilimia 52 ikiwa ni pamoja na madaktari.

Kwa upande wake, mkurugenzi mtendaji wa shirika lisilo la kiserikali linaloangazia huduma bora za afya nchini anasema ufinyu wa bajeti ambapo mwaka huu wa fedha bajeti ilikuwa ni shilingi bilioni 540 huku fedha inayotengwa ni shilingi bilioni 80 na hiyo kupelekea kuzorota kwa huduma licha ya kuongeza idadi ya madaktari………