Alhamisi , 16th Jun , 2016

Msemaji wa Chama cha Mapinduzi CCM, Christopher Ole Sendeka ametoa tamko kuhusu tuhuma zilizotolewa na Askofu Josephat Gwajima kuhusana na suala la Uenyekiti wa CCM.

Bila ya shaka mmepata habari kupitia mitandao ya kijamii na vyombo vya habari kuwa siku ya Jumapili ya tarehe 11/06/2016 akiwa kanisani kwake, Mchungaji Josephat Gwajima wa Kanisa la Ufufuo na Uzima alitoa kauli za uongo, uchochezi na uchonganishi dhidi ya Chama cha Mapinduzi, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi Dkt Jakaya Mrisho Kikwete, Rais wa Jamhuri ya Muungano Dkt. John Pombe Magufuli, Viongozi wa CCM, Watendaji wa CCM na Serikali ya Awamu ya nne.

Mchungaji Gwajima amedai ati kwamba lipo kundi la wanaCCM wanaozunguka sehemu mbalimbali za nchi wakishawishi wanachama na wakimshawishi Mwenyekiti wa sasa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete ili aendelee na Uenyekiti na kuleta hoja ya kutenganisha kofia ya Uenyekiti wa CCM na Urais wa nchi.

Napenda kuwafahamisha wana CCM, wapenzi wa CCM na wananchi kwa jumla kuwa madai hayo ya Mchungaji Gwajima ni uongo mtupu na hayana hata chembe ya ukweli. Ni mambo ya uzushi na hadithi ya kufikirika amesema Christopher Ole Sendeka. Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi CCM.

Kwa upande mwingine Shirikisho la Wanafunzi wa Vyuo vya Elimu ya Juu Tanzania limeshitushwa na taarifa za uchochezi zilizotolewa na kiongozi wa dini wa kanisa la Ufufuo na Uzima hivi karibuni likituhumu viongozi wa Chama cha Mapinduzi kuwa na mipango ya kutokumkabidhi Chama Raisi wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. John Joseph Pombe Magufuli.

Tunatoa rai kwa viongozi na Taasisi za kidini zote nchini kutojihusisha na masuala ya kisiasa na badala yake kutekeleza majukumu yaliyokusudiwa kwa uwepo wao. Kuhusisha siasa na dini ni kuchochea uhasama na kupandikiza mbegu za chuki, vurugu, uchochezi na kuhatarisha uvunjifu wa amani baina ya wananchi, viongozi na Taifa kwa ujumla. Hivyo hatuko tayari kuwavumilia watu wote wenye nia ya kutuvurugia amani tuliyo nayo na kutuingiza kwenye migongano ya kidini.

Mwisho tunapenda kuiomba serikali kupitia vyombo vya dola kushughulikia kwa kina jambo hili na kulichukulia hatua ili kukomesha vitendo vya uchochezi baina ya watanzania na baina ya viongozi.