Ameyasema hayo (Ijumaa, Februari 16, 2024) wakati akitoa hoja ya kuahirisha Bunge, ambapo amesema ujenzi wa shule hizo uliwezesha watoto wengi waliofaulu elimu ya msingi kujiunga na elimu ya sekondari na alitilia mkazo suala la elimu na kupiga vita mimba kwa wanafunzi.
Amesema suala lingine ni kurasimisha biashara ya pikipiki (Bodaboda)kubeba abiria jambo ambao limesaidia vijana kupata ajira, kusimamia uanzishwaji wa SACCOS nchini pamoja na kubadili Vyuo vya Ualimu vya Mkwawa na Chang’ombe ili viwe vyuo vikuu vya ualimu.
Katie Hatua nyingine, Mheshimiwa Majaliwa amewataka Watanzania wote bila kujali itikadi za kisiasa, kidini na kikabila washiriki kikamilifu kutoa maoni ili kuhakikisha Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo inakuwa jumuishi na shirikishi.
Pia, Waziri Mkuu amewataka viongozi wa Mikoa, Wilaya, Halmashauri, Kata/Shehia, Mitaa/Vijiji na vitongoji wahamasishe na kuwaelimisha wananchi wanaoishi katika maeneo yao ili washiriki kikamilifu katika kutoa maoni ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo.
Kadhalika, Waziri Mkuu amesema kuwa sekta binafsi asasi za kiraia, makundi maalum kama vile vijana, wanawake, wazee, watu wenye ulemavu na mashirikisho mengine yashirikiane na Tume ya Mipango katika uratibu wa ukusanyaji wa maoni ya wanachama na wadau wao. ”Hii itasaidia kuhakikisha kuwa maoni ya makundi husika yanapokelewa na kujumuishwa katika maandalizi ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo.”
Waziri Mkuu amesema kazi zinazofuata katika maandalizi ya Dira mpya ya Taifa ya Maendeleo ni pamoja na kutoa elimu kwa umma kupitia kampeni ya kitaifa ya uhamasishaji wananchi kushiriki katika maandalizi ya Dira mpya na kukamilisha na kusambaza taarifa ya ukusanyaji maoni.