Jumatatu , 3rd Oct , 2016

Taasisi ya Taifa ya Utafiti wa Magonjwa ya Binadamu NIMR, imesema kuwa tafiti zinazofanywa na taasisi za utafiti zinasaidia serikali katika sekta ya Afya ikiwemo kupunguza mlipuko wa magonjwa mbalimbali yakiwemo yasiyopewa kipaumbele.

Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Taifa ya Utafiti Magonjwa ya Binadamu Dk Mwele Malecela.

Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Taasisi hiyo Dkt. Mwele Malecele amesema tafiti zao zimesaidia kwa kiasi kikubwa ikiwemo kufuta kabisa ugojwa wa matende katika baadhi ya maeneo, usubi, kichocho pamoja na minyoo ya tumbo.

Dkt. Malecela amesema taasisi hiyo kwa kushirikiana kwa ukaribu na Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, wameweza kupeleka kwa karibu vituo vya huduma za afya katika maeneo ambayo walikuwa wanakosa huduma hizo.

Mkurugenzi huyo amesema kuwa wanategemea kutokomeza magonjwa yasiyopewa kipaumbele ikiwemo magonjwa ya matende na mabusha, kichocho, minyoo ya tumbo na usubi ambapo mpaka sasa wamepiga hatua kubwa katika baadhi ya maeneo.