Ijumaa , 9th Oct , 2015

Mtandao wa waangalizi wa Uchaguzi nchini TACCEO wameitaka taasisi ya kupambana na kuzuia rushwa nchini ( PCCB) kuongeza nguvu katika kuhakikisha wanakemea na kuzuia vitendo vya rushwa katika kampeni zinazoendele hapa nchini.

Kaimu Mwenyekiti wa TACCEO Wakili, Imelda Lulu Urio

Akiongea na waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam wakili Imelda Urio amesema katika majimbo 200 ambayo TACCEO wameweka waangalizi wamebaini kuwa kuna viashiria vingi vya Rushwa na kampeni za usiku za nyumba kwa nyumba zenye viashiria vingi vya ukiukaji wa maadili ya uchaguzi.

Wakili Urio ameongeza kuwa tume ya uchaguzi ni lazima ivikanye vyama vya siasa kuacha kuwatumia watoto wadogo katika kampeni zao kwani wanawaweka watoto katika mazingira hatarishi ambapo ni kinyume na sheria ya watoto na haki za binadamu.

Aidha TACCEO imezitaka taasisi za umma kuacha kutumia mali za serikali kama magari katika uchaguzi kwani ni kinyume na maadili na sheria za uchaguzi.