Alhamisi , 14th Jul , 2016

WAZIRI wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Prof. Makame Mbarawa ameiagiza Mamlaka ya Viwanja vya Ndege Tanzania -TAA kuongeza kiwango cha ukusanyaji mapato kutoka Bilioni 74 hadi kufikia bilioni 105 katika mwaka wa fedha 2016/2017.

Profesa Mbarawa ametoa agizo hilo Jijini Dar es Salaam wakati akizungumza na wafanyakazi wa Mamlaka hiyo mara baada ya kukagua majengo matatu na ofisi mbalimbali zilizopo Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere -JNIA.

Profesa Mbarawa amewasisistiza wafanyakazi wa Uwanja huo kuhakikisha kiasi cha ukusanyaji wa mapato hayo kinaongezeka siku hadi siku ili kukuza uchumi wa taifa na kuchochea fursa za kimaendeleo.

Aidha, katika ziara hiyo Waziri Profesa Mbarawa alibaini ucheleweshwaji wa vibali kwa abiria wanaoingia katika Uwanja wa Ndege wa JNIA ambapo abiria huchukua zaidi ya saa moja kupata vibali vyao hali inayoleta picha mbaya kwa wageni wanaoingia nchini.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa TAA, mhandisi George Sambali amemhakikishia Profesa Mbarawa kuwa mapungufu yaliyobainishwa yatafanyiwa kazi ili kuongeza ufanisi na huduma bora kwa abiria.