Mkuu wa Mkoa wa DSM, Paul Makonda akikabidhi majina ya watuhumiwa kwa Kamishna Mkuu Rogers Sianga
Sianga aliyeapishwa jana na Rais Magufuli, ametoa tamko hilo leo wakati kupokea kijiti kutoka kwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Bw. Poul Makonda ikiwa ni pamoja na kukabishiwa majina ya watu 97 ya wafanyabiashara wakubwa, wanaotuhumiwa kujihusisha na dawa za kulevya.
Kamishna Sianga amesema kuna mahakimu na majaji ambao wamekuwa wakivuruga kesi za watuhumiwa wa dawa za kulevya ambapo pia amesema watapitia kesi zote za madawa ya kulevya ili kuwabaini na kisha watapeleka orodha kamili katika mamlaka husika ili hatua zichukuliwe.
Akitolea mfano wa kesi ambazo amedaia zilivurugwa na mahakimu, amesema kuna kesi moja ambapo ushahidi ulikuwa wazi kuwa mtuhumiwa amemeza dawa za kulevya, lakini hakimu akasema kuwa mtuhumiwa huyo alikuwa na matatizo ya vidonda vya tumbo.
Pia Sianga ameagiza kukamatwa kwa maafisa wa polisi waliosaidia kuingiza viwatilifu vya kutengeneza dawa za kulevya nchini kiasi cha takriban tani 21.
Paul Makonda
Naye Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Mhe Poul Makonda amesema katika mkoa huo kuna bandari bubu 54 huku 27 zikiwa zinatumika kupitishia dawa za kulevya.
Pia amesema kuna takriban nyumba 200, hoteli 67, Club 20 na vijiwe 107 vinavyotumika kusambaza na kuuza dawa za kulevya huku akibainish kuwa kwa utafiti alioufanya, kila siku katika jiji hilo, kati ya kila 10 hadi 15 husambazwa na kumalizika kila siku.
Mkutano huo wa mapambano ya dawa za kulevya uliofanyika kwenye ukumbi wa Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam ulihudhuriwa pia na viongozi wa kidini, wanasiasa, wabunge, madiwani, wakuu wa idara mbalimbali katika halmashauri za mkoa wa Dar es Salaam, wadau mbalimbali wa mapambano ya dawa za kulevya pamoja na waathirika wadawa za kulevya.