Kifungu ambacho sasa kinapingwa kwa nguvu kupitia kesi ya kikatiba, iliyofunguliwa na Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), na mashirika mengine ni kifungu cha 16, ambapo mmoja kati ya mawakili wa shauri hilo Jebra Kambole anadai kuwa kifungu hicho hakifai kwa kuwa kinaweza kumuingiza kila mtanzania matatani.
Amesema kifungu hicho kinahusu mtu anayeweka taarifa za uongo mitandaoni, na kwamba ndicho ambacho kimewakamatisha watu wengi wenye kesi mahakamani kwa hivi sasa.
Kifungu hicho cha 16 kinasema:-
"Mtu atakayechapisha taarifa au data katika picha, maandishi, alama au katika namna nyingine yoyote katika mfumo wa kompyuta, akijua kwamba taarifa au data ni za uongo, zinapotosha, zisizo sahihi, na kwa lengo la kudhalilisha, kutishia, kutusi au kwa naamna nyingine kudanganya umma au kuchochea utendaji wa kosa, atakuwa ametenda kosa, na akipatikana na hatia atalipa faini isiyopungua shilingi milioni tano au kutumikia kif
ungo kisichopungua miaka mitatu au vyote kwa pamoja".
Katika shauri hilo upande wa Jamhuri uliweka pingamizi la awali la kutosikilizwa kwake, na kinachosubiriwa ni maamuzi ya mahakama juu ya shauri hilo.
Wakili Jebra anasema ana matumaini makubwa kuwa kifungu hicho kitabatilishwa huku akishangilia maamuzi yaliyofanywa na mahakama katika shauri lingine ya kuiamuru serikali kukifanyia marekebisho kifungu cha 50 cha sheria hiyo.
Wakili Jebra Kambole
Katika shauri hilo ambalo mahakama ilitoa maamuzi mwishoni mwa mwezi Desemba , 2016 Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) ameondolewa mamlaka ya kutoa adhabu isiyokatiwa rufaa kwa mshtakiwa anayekiri makosa ya kimtandao.
Uamuzi huo ulitolewa na Mahakama Kuu na kuipa Serikali miezi 12 kukifanyia marekebisho kifungu hicho ambacho kinasema
Kubatilishwa kwa kifungu hicho, kinamfanya wakili Jebra Kambole kupata usingizi mzito, ambapo amesema hatua hiyo ni ya kihistoria, kwani haijawahi kutokea sheria ikatungwa halafu ndani ya mwaka mmoja ikaonekana kuwa na mapungufu na kutakiwa kufumuliwa.
Mahakama hiyo imetoa maelekezo kwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali kufanya marekebisho kwenye kifungu hicho (kifungu cha 50) kimoja kati ya vifungu takriban 21 vya sheria hiyo vilivyokuwa vikilalamikiwa kwa vile kifungu hicho kinakiuka haki ya msingi ya mwananchi ya kusikilizwa.
Vifungu vingine vilivyokuwa vikilalamikiwa ni pamoja na 4, 5, 6, 7, 8, 9, 10, 11, 14, 19, 21, 22 , 31, 32, 33,34 35, 35, 37, 38 na 50 ambapo maada ya mahakama kujirisha kuwa haviendi kinyume na katiba, imeamua kuvihalalisha.
"Uzuri katika vipengele ambavyo mahakama imehalalisha hakuna kipengele cha 16 ambacho ndio mwiba, tunafanyia kazi na huenda tukakata rufaa, cha hamsini kwetu ni usingizi mkubwa sana" Amesema Wakili Jebra




