Serikali yazipiga marufuku halmashauri

Saturday , 18th Nov , 2017

Serikali imepiga marufuku halmashauri zote nchini kuingia makubaliano na mashirika yasiyokuwa ya kiserikali(NGO’S) bila kupitia na kuidhinishwa na Ofisi ya Rais, Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa( TAMISEMI ).

Kauli hiyo imetolewa mjini Tabora na Naibu Katibu Mkuu (ELIMU) Ofisi ya Rais, Serikali za Mitaa na Tawala za Mikoa (TAMISEMI) Tixon Nzunda wakati akizungumza na watendaji  na watumishi wa Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tabora.

Nzunda amesema kwenye baadhi ya NGO’s mambo yamekuwa hayaendani na vipaumbule vya serikali ambavyo ni kuwasaidia wananchi badala yake NGO’s zimekuwa zinakwenda tofauti na kujinufaisha zenyewe.

Ameongeza kuwa kabla ya kuanza utekelezaji wa shughuli za NGO’s ni vyema halmashauri zikapeleka (TAMISEMI) maombi ya mashirika ambayo yameomba kufanyakazi katika maeneo yao ili serikali ione kama kweli inaendana na vipaumbele ambavyo imepanga katika kuboresha maisha ya watanzania ambao maisha yao yako chini.

Aidha ameeleza Mashirika ambayo yana nia ya kweli ya kusaididia watanzania lazima yakubaliane na vipaumbele vya serikali ili yaweze kufanya kazi nchini vinginevyo ni vyema yakatafute nchi nyingine ya kufanya mambo yake bila kufuata utaratibu wa nchi husika.

Naibu Katibu Mkuu huyo yupo katika ziara ya kikazi katika Mikoa ya Kigoma, Tabora na Singida kwa lengo ya kuhimiza usimamizi bora wa sekta ya elimu, kilimo, mifugo na utawala bora.