
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola.
Akizungumza leo Agosti 29, 2018 katika wiki ya Jeshi la Zimamoto katika uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Kangi Lugola amesema ajira hizo zitaongeza kasi ya kukabiliana na majanga ya moto yanayojitokeza maeneo mbalimbali nchini.
“Tunatambua changamoto ya upungufu wa wafanyakazi katika kikosi hiki hivyo tutaajiri watumishi 1,500 ili kuongeza nguvu iliyopo,” amesema Lugola.
Katika hatua nyingine, Lugola amewaagiza wakurugenzi wote wa majiji pamoja na miji kutoruhusu ujenzi holela na badala yake wazingatie mipango miji kwa sababu unasababisha vikosi vya zimamoto kushindwa kufika eneo la tukio kwa wakati.
Kamishna Jenerali wa jeshi hilo, Thobias Andengenye amesema wanakabiliwa na uhaba wa wafanyakazi ikilinganishwa na ukubwa wa nchi na idadi ya wananchi na kutaja changamoto nyingine kuwa ni upungufu wa magari katika ofisi za mikoa na wilaya na kupendekeza magari 100 yatasaidia kufanya kazi kwa urahisi.
Agosti 19 magari saba ya mizigo yaliteketea kwa moto katika kituo cha forodha Rusumo wilaya ya Ngara, mpakani mwa Tanzania na Rwanda, baada ya gari moja la mafuta ya petroli kuligonga gari jingine hali iliyopelekea Helkopta ya jeshi la Rwanda kusaidia kuzima moto ulioteketeza shehena iliyokuwa imepakiwa na magari hayo baada ya kukosekana kwa magari ya zimamoto wilayani humo.