Alhamisi , 20th Feb , 2025

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel, amesema kwamba serikali imeendelea kuhakikisha huduma za upatikanaji wa dawa (ARV) za kufubaza makali ya Virusi vya UKIMWI zinaendelea kupatikana bila malipo kwa wagonjwa wote.

Naibu Waziri wa Afya Dkt. Godwin Mollel

Kauli hiyo ameitoa hii leo Februari 20, 2025 alipoungana na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Bunge na Uratibu) Ummy deriananga, na viongozi wengine na wadau katika uzinduzi wa awamu ya tatu ya Mradi wa Timiza Malengo uliofanyika mkoani Lindi.

Dkt Mollel amesema serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imeboresha sekta ya afya kwa kiasi kikubwa ikiwemo ujenzi wa miundombinu ya afya ambapo serikali imetumia kiasi cha zaidi ya bilioni 48 kwenye ujenzi wa miundombinu peke yake kama vile hospitali, vituo vya afya na zahanati katika mkoa wa Lindi.

Dkt Mollel akizungumzia upatikanaji wa huduma za afya za kibingwa amesema, "Hapo mwanzo zilikuwa hazipatikani katika nchi yetu lakini kwa sasa zipo Tanzania, mfano matibu ya uvumbe wa ubongo bila kupasua kichwa sambamba na matibabu ya kansa ya ubongo kwa kutumia sauti maalumu,".

Mradi wa TIMIZA MALENGO awamu ya tatu unatekelezwa katika halmashauri 36 katika mikoa 10 ya Tanzania Bara ambayo ni Dodoma, Geita, Lindi, Mara, Morogoro,Njombe, Ruvuma, Singida,Tabora na Tanga.