Jumanne , 19th Jun , 2018

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, jinsia, Watoto na Wazee, Ummy Mwalimu amesema Serikali itaanza kutoa dawa mpya za kupunguza makali ya Virusi vya Ukimwi (ARVs) itakayokuwa na ufanisi zaidi kuliko inayotumika hivi sasa nchini.

Ummy ameyasema hayo leo katika uzinduzi wa kampeni ya Furaha Yangu, Pima, Jitambue, Ishi, inayolenga kuhamasisha wananchi hasa wanaume kupima VVU kwa hiari na kuanza matumizi ya dawa za kufubaza makali ya ugonjwa Ukimwi (ARVs)

“sasa hivi mtu yeyote atakayekutwa na maambukizi ya VVU nchini ataanzishiwa dozi mapema ili kupunguza makali na kukinga maambukizi mapya ili kufikia lengo la mapambano dhidi ya ugonjwa huo hasa kwa wanaume ambao ndio kundi lenye uzito wa kupima afya”, amesema Waziri Ummy.

Amesema mpango huo wa kutoa dawa kwa miezi mitatu hautawahusu wajawazito, watoto na wale ambao mwenendo wao wa utumiaji ARVs hauridhishi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akikata utepe kuashiria uzinduzi wa kampeni ya kitaifa ya kupima Virusi vya UKIMWI (VVU) na kuanza kutumia dawa mapema inayojulikana kama Furaha Yangu iliyofanyika katika uwanja wa Jamhuri, Jijini Dodoma leo.

Ummy amesema pia wamepanga kuongeza vituo vya kutoa huduma kwa watu wanaoishi na VVU ambapo hadi kufikia Desemba mwaka huu vitafikia 4,050 kutoka 1,866 vilivyopo sasa