Jumatatu , 27th Apr , 2020

Serikali imetolea ufafanuzi kuhusu Idara ya Uhamiaji nchini Zambia kuwazuia madereva wa IT katika mpaka wa Tunduma Mkoani Songwe kuingia nchini Zambia, ikiwa ni katika kujikinga na Virusi vya Corona.

Kituo cha ukaguzi mpakani mwa Tanzania na Zambia

Mkuu wa Wilaya ya Momba mkoani Songwe, Juma Said Irando ambaye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama, ametolea ufafanuzi wa malalamiko ya madereva hao wa IT waliokwama mpakani kwa takribani wiki mbili sasa.

"Mpaka wa Tunduma unahudumia nchi mbili, watumiaji wa mpaka huu wafuate utaratibu unaotakiwa kulingana na sheria za nchi zote mbili, Tanzania ina sheria zake na wale wanaokwenda nchi ya pili kule wafuate sheria zake" amesema Mkuu huyo wa Wilaya.

"Tukifuata sheria za nchi zote mbili tutaishi kwa wema na amani na kudumisha mahusiano yetu yaliyodumu kwa muda mrefu sasa", ameongeza.

Awali madreva hao waliiomba serikali ya Tanzania kuingilia suala hilo ili kumaliza utata wa changamoto wanazokutana nazo .

Aidha uongozi wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) umesema, utatoa muongozo kuhusu msamaha wa faini kwa madereva watakaokaa karantini siku 14 wakati nyaraka zikiwataka kuvuka mpakani ndani ya siku 7 ili kuondoa usumbufu.