Jumatatu , 18th Jan , 2016

Serikali kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi imeanza kuchukua hatua kukabiliana na changamoto ambazo zimekuwa zikichangia kwa kiasi kikubwa kushuka kwa kiwango cha ufaulu na kuporomoka kwa elimu kwa shule za msingi.

Mkurugenzi wa sera na mipango wa wizara ya Elimu, Sayansi,Teknolojia na Ufundi Clifford Tandari

Akifunga mafunzo ya mradi wa elimu nchini katika kituo cha Bunda,Mkurugenzi wa sera na mipango wa wizara hiyo Bw. Clifford Tandari,amesema hatua ambazo zimeanza kuchukuliwa na serikali kupitia mpango wa matokeo makubwa sasa ni pamoja na kutoa mafunzo maalum kwa walimu wa masomo ya hisabati, kiingereza na kiswahili lengo ni kuinua ufaulu kwa masomo hayo kwa shule za msingi.

Kwa mujibu wa mamlaka ya elimu nchini, ambayo ndiyo inayowezesha mradi huo mkubwa, tayari kiasi cha shilingi bilioni mbili na milioni mia tatu kimetumika kwaajili ya kuwezesha mafunzo wezeshi kwa walimu na wanafunzi katika kuinua kiwango hicho cha ufaulu kwa masomo hayo kwa shule za msingi.

Tayari walimu wawezeshaji 900 wamepata mafunzo hayo ya awamu ya pili katika vituo vinane nchini ambao watatumika pia kutoa mafunzo kwa walimu elfu kumi na tano wa masomo hayo nchini kote.