Jumatatu , 1st Dec , 2014

Serikali ipo kwenye mchakato wa kukamilisha uundwaji wa mfuko maalumu wa UKIMWI  (Trust Fund) kwa lengo la kuboresha huduma za UKIMWI zinazotolewa na pia kupunguza utegemezi wa wahisani katika na kuongeza kasi ya mapambano dhidi ya UKIMWI.

Akihutubia umati wa wakazi wa mkoa wa Njombe na mikoa jirani katika maadhimisho ya siku ya UKIMWI duniani iliyofanyika kitaifa mkoani njombe  makamu wa Rais wa jamhuri ya muungano Dkt Mohammed Gharib Bilal amesema kazi ya kupambana na ugonjwa huo ni ya kila mwanachi hivyo kila mmoja anapaswa kuwajibika kwa nafasi yake ambapo amewaomba wadau kutoka nje na ndani ya nchi kuchangia mfuko huo.

Dk Bilal ameongeza kuwa kutokana na baadhi ya mikoa kuwa na wastani wajuu zaidi ya wastani wa kitaifa ikiongozwa na mkoa wa Njombe wenye wastani wa asilimia 14.8 serikali itaendelea kuwekeza nguvu katika kuelimisha umma juu ya namna ya kujikinga na maambukizi ya UKIMWI bila kuonea aibu suala hilo…

Kwa upande wake Naibu Waziri wa Elimu TAMISEMI Kassim Majaliwa aliyemwakilisha waziri wa afya na ustawi wa jamii Dkt. Seif Rashid amesema wizara hiyo itaendelea kuunga mkono juhudi za wadau wanaoshiriki mapambano dhidi ya UKIMWI ikiwa ni pamoja na kuendelea kutoa huduma za dawa za kufubaza virusi vya UKIMWI bure kwa wote wanaoishi na virusi hivyo.

Naye Mwenyekiti wa shirikisho la vyama vya watu wanaoishi na virusi vya UKIMWI bwana Julius Kaaya ameitaka serikali kukemea dhihaka inayofanywa na baadhi ya viongozi wa kisiasa kwa watu wenye virusi vya UKIMWI.

Mkuu wa mkoa wa Njombe Dokta Rehema Nchimbi amesema kutokana na juhudi zinazofanywa na mkoa huo kupunguza maambukizi mapya ya virus vya UKIMWI dalili zimeanza kutoa matumaini ya kupungua kwa maambukizi hayo kwa kutumia takwimu za watu waliojitokeza kupima UKIMWI kwa siku za karibuni.

Tags: