Jumatatu , 3rd Oct , 2016

Serikali inafanya mapitio ya sera mbalimbali zinazohusiana na masuala ya nyumba nchini, yenye lengo la kuweka mfumo wezeshi ambao utarahisisha uendelezaji wa sekta ya nyumba na kuisaidia kuweza kuendelea kufanya vizuri.

Waziri wa Ardhi, Mheshimiwa William Lukuvi. (Kushoto)

Sera zinazofanyiwa mapitio ni pamoja na sera ya ardhi ya mwaka 1995 na sera ya taifa ya maendeleo ya makazi ya mwaka 2000.

Kauli hiyo imetolewa leo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi Mhe. William Lukuvi alipokutana na wadau wa masuala ya ardhi wakati leo Tanzania ikiungana na nchi nyingine duniani kuadhimisha Siku ya Makazi Duniani.

Amesema wizara ya ardhi ipo kwenye hatua za awali za kuandaa muswada wa sheria ya uendelezaji milki ambayo utasaidia kupunguza makazi holela, na kutoa mwongozo wa kuratibu na kusimamia haki za wawekezaji na wapangaji na kusimamia ubora wa majengo na huduma zake.

Kwa upande wa wadau na waendeleza ardhi nchini wamesema katika kuhakikisha wanasaidia taifa kuepuka ujenzi holela wameweka mikakati maalum ya kusaidia sekta ya ardhi kuimarika nchini.

Umoja wa Mataifa uliipitisha na kuitenga kila Jumatatu ya kwanza ya mwezi Oktoba kila mwaka kuwa ni siku maalum kwa maadhimisho ya Siku ya Kimataifa ya Makazi.

Kauli mbiu ya Siku ya Makazi Duniani ni NYUMBA KITOVU CHA MIJI, kauli ambayo inasimamia usalama wa umiliki wa ardhi, upatikanaji wa huduma, vifaa na miundombinu, uwezo wa kumudu gharama za nyumba, kukalika, kufikika, mahali na utoshelevu wa kitamaduni.

Inakadiriwa ifikapo mwaka 2050 nusu ya wakazi wote duniani watakua wakiishi mjini.