Jumatano , 30th Mar , 2016

Serikali ya Tanzania imesema imepokea ripoti kutoka kwa wakuu wa Mikoa yote 26 ya Tanzania Bara kuhusu kuondolewa kwenye malipo ya watumishi hewa ambayo yalikuwa yakiiingizia serikali hasara ya mabilioni ya shilingi.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe. George Simbachawene.

Akizungumza na Waandishi wa Habari jana Jijini Dar es Salaam Waziri wa nchi Ofisi ya rais TAMISEMI, Mhe. George Simbachawene amesema kuwa kuwasilishwa kwa ripoti hiyo ni utekelezaji wa agizo la rais kutaka watumishi hewa waondolewe.

Simbachawene amesema kuwa jana ndio ilikuwa ni siku ya mwisho ya utekelezaji wa agizo hilo na kwamba wakuu wote wa mikoa wamelitekeleza kama walivyoagizwa.

Waziri huyo wa Tamisemi amesema kuwa kwa sasa taarifa hizo zinakusanywa kwa pamoja ili kupata idadi kamili na zitakapokuwa tayari kwa matumizi ya umma zitatolewa kwa vyombo vya habari kwa lengo la kufahamisha umma.