
Akizungumza na vyombo vya habari nchini Mke wa Raphael Ongangi amesema amezungumza na mume wake kwa njia ya simu akitokea nchini Kenya ikiwa ni siku chache tangu achukuliwe na watu wasiojulikana Juni 24, 2019.
"Raphael amepatikana Mombasa Kenya, na yupo salama salimini sina taarifa nyingine zaidi ya hiyo ila hiyo inatosha sana kwangu" amesema Veronica
Mapema leo Waziri wa Nchi Ofisi ya Raisi Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala bora, George Mkuchika amesema kwa sasa hana majibu yoyote juu ya madai ya Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe juu ya Waziri huyo kutofuatilia taarifa alizopewa na Mbunge huyo kupotea kwa raia wa Kenya Raphael Ongangi.
Waziri Mkuchika ametoa kauli hiyo wakati akizungumza kwenye East Africa Breakfast cha East Africa Radio, wakati alipoulizwa kuhusiana na madai ya Mbunge Zitto ambaye alimtaja Waziri huyo kuwa hakupata msaada wowote alipowasilisha suala la kupotea kwa Raphael.
"Kuhusiana na madai ya Zitto Kabwe kwa sasa siwezi kusema chochote, kwa sababu sijamsilikiliza na sijui hoja yake ni nini, kuhusu mimi kupokea taarifa yake juu ya kupotea kwa Raphael kwa kifupi siwezi kujibu chochote kuhusu hilo." amesema Mkuchika
Mapema jana akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es salaam Mbunge wa Kigoma Mjini alieleza kufanya jitihada mbalimbali za kuhakikisha mfanyabiashara Raphael Ongangi lakini ziligonga mwamba.
"Nilipokuwa Dodoma niliwasiliana na Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na Waziri Mkuchika kuhusiana na kupotea kwa Raphael, lakini mpaka leo sijapata taarifa yeyote na tayari siku 7 zimeshapita. " alisema Zitto