Jumatano , 7th Jul , 2021

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewataka watanzania kulinda amani walionayo na kutokuunga mkono mambo yanayolenga kudhoofisha amani ya nchi.

Rais Samia ametoa kauli hiyo leo akiwa njiani  Morogoro ambapo amekiri uwepo wa vichokochoko nakuwataka watanzania wasiingie mkenge kwani familia zao ndizo zitakazoathirika. 

“Niwaombe sana ndugu zangu vijichochoko vimeanza, naomba msivipokee, wanaokuja na vijichokochoko walishajua matumbo yao yanajaaje pesa za matibabu wanatoa wapi nawaomba sana wasije wakawaingiza kwenye huo mkenge,” amesema Rais Mhe. Samia.

"Pakichafuka ni wewe utakaye kaa ndani na watoto wako na mama watoto na msijue chakula wanatoa wapi, niwaombe sana tulinde amani yetu nchi yetu itulie tuendelee na maendeleo yetu,” ameongeza Rais Mhe. Samia.

Pia Rais Samia ameiomba serikali kuyagawa mashamba yaliyofutwa umiliki Kilosa kwa wananchi na mengine kubakishwa kwa ajili ya kilimo kikubwa cha uwekezaji.

Rais Samia ametokea Dodoma hivi leo akielekea Morogoro  ambapo anatarajia kuhudhuria  mkutano unaotarajiwa kufanyika kesho ndani ya mkoa huo.