Jumanne , 28th Jul , 2020

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Magufuli, leo akihutubia Taifa wakati wa shughuli za mwisho za kuaga mwili wa Rais Mstaafu Benjamin Mkapa, alimwaga machozi wakati akikumbuka ni kwa namna gani alikuwa akimsaidia wakati wa uhai wake na kuomba watu wasimshangae kisa analia.

Rais Magufuli akiwa na Hayati Benjamin William Mkapa,wakati wa uhai wake.

Wakati wa Hotuba yake Rais Magufuli hii leo Juali 28, 2020, ameeleza mafanikio makubwa, yaliyopatikana kwa Taifa mara tu baada ya Rais Mkapa kuingia madarakani, ikiwemo suala la kukuza uchumi na kupunguza madeni ambayo nchi ilikuwa ikidaiwa na Mataifa pamoja na Mashirika ya nje.

"Mzee Mkapa alinilea kama Mtoto wake, alikuwa ni shujaa wangu, alinionesha upendo, saa nyingine machozi yanakuja tu msinishangae sana, hata Mzee Kikwete nilimuona juzi anadondosha machozi tena Kikwete ni Kanali ila alitoa chozi kwahiyo msinishangae shnagae sana unajua kifo saa nyingine hauwezi kukivumilia, nasema kweli wakati wote alikuwa akinionesha upendo mkubwa sana, kuondoka kwake ni pigo kubwa kwangu" amesema Rais Magufuli.

Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin William Mkapa, alifariki Dunia usiku wa kuamkia Julai 24, 2020, kutokana na tatizo la mshituko wa moyo na atazikwa siku ya kesho Julai 29, 2020, katika Kijiji cha Lupaso, Masasi mkoani Mtwara.