Alhamisi , 9th Apr , 2015

Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa Tanzania Peter Kuga Mziray amesema mwenendo wa Tume ya Uchaguzi kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura hauridhishi na unatoa viashiaria vya uwezekano wa kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu mwezi Oktoba.

Mwenyekiti wa Baraza la vyama vya siasa Tanzania Peter Kuga Mziray amesema mwenendo wa Tume ya Uchaguzi kuboresha daftari la kudumu la wapiga kura hauridhishi na unatoa viashiaria vya uwezekano wa kuahirishwa kwa uchaguzi mkuu mwezi Oktoba na kuwaongezea muda viongozi waliopo akiwemo Rais Kikwete.

Mziray amesema kuwa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) katika suala la uboreshaji wa daftari la wapiga kura na upigaji kura ya maoni imeshindwa kufanya kazi yake na hivyo inatakiwa kuachia ngazi mara moja.

Mziray ambaye pia ni mwenyekiti wa chama cha APPT-Maendeleo amesema hayo leo wakati akiwa katika kipindi cha HOT MIX cha EATV ambapo amedai kuwa tume hiyo ilijua tangu zamani kuwa kufikia mwaka huu daftari lilipaswa kuwa limeboreshwa lakini lakini cha kushangaza hadi sasa kazi ya uboreshaji haina matumaini yoyote kama itamalizika kwa wakati.

“Kwa mujibu wa ratiba ya Tume, mwezi wa nane mwaka huu ni kipindi cha wagombea kuanza kuchua fomu za urais, sasa itamaliza kazi hiyo lini? Inasema mwezi wa saba lakini hiyo haiwezekani, hii inaweza kuwa ni janja ya kuwaongezea viongozi waliopo muda kwa njia ya kuahirisha uchaguzi” amesema Peter Mziray.

Amesema Baraza la Vyama vya Siasa na chama chake cha APPT – Maendeleo haviko tayari kuona Rais Kikwete akiongezewa muda, jambo la msingi ni viongozi wote wa tume kujiuzulu nafasi zao kwa kuwa wameshindwa kufanya kazi yao kwa wakati.

Kuhusu hatma ya katiba mpya, amesema kuwa ni vyema serikali ifanyie marekebisho katiba iliyopo ya mwaka 1977 katika maeneo ambayo Kituo cha Demokrasia na Rais Kikwete walikubaliana ambayo ni pamoja na kuwepo tume huru ya Uchaguzi, Matokeo ya uchaguzi wa Rais kupingwa mahakamani na kuwepo kwa mgombea huru .