Jumatano , 3rd Jul , 2024

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anasisitiza ufanyaji kazi kwa ushirikiano kati ya serikali na taasisi za dini nchini ili kuendelea kujenga amani, umoja na mshikamano.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, akiwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Wolfgang Pisa

Amesema kuwa serikali inatambua mchango mkubwa unaotolewa na taasisi hizo ambao huleta matokeo chanya kwa ustawi wa Taifa.

Amesema hayo wakati akiwasilisha Salamu za Pongezi kutoka kwa Rais Dkt. Samia leo (Jumatano, Julai 03, 2024) kwa Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) Mhashamu Wolfgang Pisa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi, kwenye makazi ya Askofu, Mtanda mkoani Lindi.
 
"Tunashukuru tunapata ushauri, yapo mambo ambayo mnayafanya na kuiwezesha nchi hii iendelee, mshikamano wetu ndani ya nchi, umoja wetu ndio unaozaa utulivu na amani tuliyonayo," amesema Waziri Mkuu
 
Amesema kuwa serikali itaendelea kumpa ushirikiano wa dhati "wakati wote utakapokuwa na jambo ambalo unadhani serikali inahitaji kushauriwa uwe huru na wakati wote unapoona kwamba unahitaji kuunganisha nguvu na serikali, sisi tutakupa ushirikiano”
 
Kwa upande wake Askofu Pisa amemshukuru Rais Dkt. Samia Kwa salamu za pongezi za kuchaguliwa kwake kuwa Rais wa TEC.
 
Uchaguzi wa viongozi wapya wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC) uliohusisha nafasi za Rais, Makamu wa Rais na Katibu ulifanyika tarehe Juni 21, mwaka huu, ambao waliochaguliwa ni Mhashamu Wolfgang Pisa Askofu wa Jimbo Katoliki la Lindi (Rais), Mhashamu  Eusebius Nzigilwa Askofu wa Jimbo Katoliki la Mpanda (Makamu wa Rais) na Padre Charles Kitima Padre wa Jimbo Katoliki la Singida (Katibu Mkuu).