Jumamosi , 2nd Mar , 2024

Jeshi la Polisi mkoani Iringa limetolea ufafanuzi taarifa za kifo cha kijana Martin Chacha ambaye taarifa za kifo chake zilizua utata mitandaoni

Kamanda wa Polisi mkoani Iringa SACP Allan Bukumbi amesema kuwa kifo cha kijana huyo ambaye alikuwa ni dereva katika kampuni ya ASAS kimetokea gerezani alipokuwa anatumikia kifungo cha miezi 3 jela baada ya kupatikana na hatia ya kuiba mafuta ya diesel lita 383 

"Tumeona katika mitandao taarifa yenye kichwa cha habari, MWEKEZEJI ASAS WA IRINGA ANATUHUMIWA KUMUUWA DEREVA KWA KIPIGO AKISHIRIKIANA NA SUMA JKT"

"Taarifa hiyo inaendelea kuchunguzwa, lakini taarifa za awali ambazo ni dhahiri ni kwamba Martin Chacha Mwita alituhumiwa kuiba mafuta ya diesel lita 383 na alifikishwa Mahakamani na kesi ikasikilizwa Tarehe 20.2.2024 alipatikana na hatia na kuhukumiwa kutumikia kifungo cha miezi 3 jela" imeeleza taarifa hiyo ya jeshi la Polisi Iringa 

Polisi wamesema kuwa Tarehe 28 Februari, 2024 walipokea taarifa kutoka kwa Mkuu wa Gereza la Iringa kuhusu kifo cha mfungwa namba 47/2024 aitwaye Martin Mwita Chacha mwenye umri wa miaka 46 mkurya, mkazi wa Kunduchi Dar es salaam" 

Imeelezwa kuwa Marehemu Chacha alifariki dunia wakati akipatiwa matibabu katika hospitali ya Rufaa ya mkoa wa Iringa baada ya kuugua ghafla alipopatwa na maumivu makali upande wa moyo na kulalamika kwa wafungwa wenzake waliokuwa nae kwenye shughuli za kilimo eneo la Gereza la Mlolo na kukimbizwa hospitali haraka.
Polisi Iringa wametoa rai kwa wananchi kujiepushe na utoaji wa taarifa za uongo na upotoshaji, na kusimama kwenye ukweli na si mambo ya kuzusha kwa malengo ambayo hayatasaidia watanzania.