
Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis amekutwa na ugonjwa wa homa ya mapafu (pneumonia) katika mapafu yake yote mawili na hali yake bado "sio nzuri," inasema Vatican. Papa, mwenye umri wa miaka 88 amekuwa akipitia maambukizi ya mfumo wa upumuaji kwa zaidi ya wiki moja na amekuwa akipatiwa matibabu katika hospitali ya Gemelli huko Roma.
"Kipimo cha CT scan ya kifua ambayo Papa alifanyiwa ilionyesha kuanza kwa nimonia ya pande zote mbili, ambayo ilihitaji tiba ya ziada ya dawa," ilisema Vatican.
Vatican ilisema kwamba vipimo vya maabara na X-ray ya kifua alivyofanyiwa Papa "vinaendelea kuonyesha hali ngumu."
Hata hivyo, Vatican ilitangaza kwamba Papa bado ana "ari" na alitumia siku yake "kusoma, kupumzika na kusali."
Papa Francis pia alielezea shukrani zake kwa wale wanaomtumia salamu za pole na kuwaomba "wamuombee."
Alikuwa amepangwa kuongoza matukio kadhaa wikendi ya Mwaka Mtakatifu wa Kanisa Katoliki wa 2025, ambao utaendelea hadi Januari ijayo, hata hivyo matukio yote ya hadhara kwenye ratiba ya Papa yamesitishwa hadi Jumapili.
Katika kipindi chake cha miaka 12 akiwa kiongozi wa Kanisa Katoliki la Roma, kiongozi huyo kutoka Argentina amepatiwa matibabu hospitalini mara kadhaa, ikiwa ni pamoja na mwezi Machi 2023 alipokuwa amelazwa usiku tatu hospitalini.