Jumanne , 19th Jun , 2018

Serikali ya Tanzania imepewa angalizo na Norway ya kuweka mifumo thabiti ya uwekezaji wenye faida ukiwemo ule wa sekta ya madini, kukamilika mapema ili kuweza kutoa fursa kwa wawekezaji wapya kuwekeza kwenye sekta hiyo kwa wakati.

Kauli hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo la Norway (NORAD), Bw. Jon Lamoy wakati alipokuwa anazungumza na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dkt. Augustine Mahiga ambaye yupo nchini humo kwa ziara yake ya kikazi ya siku tatu Mjini Oslo makao makuu ya Norway.

"Jitihada za Tanzania za kupambana na rushwa, hususan kwenye ukusanyaji kodi, zitawawezesha wananchi wa Tanzania kunufaika na huduma za kijamii na hatimaye kupata maendeleo kwa haraka. Ni muhimu mkakamilisha mapema mifumo thabiti ya uwekezaji wenye faida ili kutoa fursa kwa wawekezaji wapya kuwekeza kwenye sekta ya madini kwa wakati", amesema Mkurugenzi Lamoy.

Kwa upande wake, Dkt. Mahiga amedai kuwa suala hilo tayari linafanyiwa kazi ambapo pamoja na serikali kuweka mazingira rafiki kwa wawekezaji, uwekezaji huo ni lazima uwe na faida kwa watanzania na kwa maendeleo ya nchi.

"Serikali ya Rais Magufuli imedhamiria kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati unaoongozwa na sekta ya viwanda. Katika kutekeleza hilo, serikali imepitia na kurekebisha baadhi ya sheria na mikataba ambayo ilikua inanufaisha upande mmoja", amesisitiza Dkt. Mahiga.

Kwa upande mwingine, Dkt. Mahiga amesema marekebisho yanayofanyika sasa yanalenga kwenye kuleta faida kwa pande zote mbili yaani 'win win situation'.