Jumatatu , 1st Jul , 2024

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa, amewataka wahandisi na watumishi wa Tume kuheshimu, kusimamia na kutekeleza miradi kwa viwango na ubora.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Umwagiliaji, Raymond Mndolwa

Amesema ni aibu kwa taasisi kuwa na miradi isiyokidhi viwango hivyo hatakuwa tayari kuona miradi hiyo inaiangusha serikali na Ilani ya Chama Cha Mapinduzi.

Mndolwa amesema hayo leo jijini Dodoma wakati wa kikao kazi na menejiment, wasimamizi wa miradi, wahandisi wa mikoa na wahakiki ubora wa miradi na baadhi ya watumishi.

Amesema ni muhimu kila mmoja kujua serikali inafanya kazi kubwa kuwezesha miradi hiyo kwa maslahi ya wananchi, hivyo ni muhimu usimamizi wake kuzingatia matokeo yenye ubora.

"Naomba kasimamieni miradi ni aibu kuwa na miradi isiyo na ubora, ni aibu kwenu na taasisi na tutaiangusha serikali na chama ambacho kinatutaka tutekeleze Ilani, mjue sitamuonea mtu lakini sitakuwa tayari kumvumilia yeyote asiyetekeleza wajibu wake, nitafanya mabadiliko mara kwa mara, lengo ni kuboresha utendaji na kuwa na ufanisi," amesema

Mndolwa amesisitiza umuhimu wa watumishi hao kushirikiana na Mkurugenzi wa Rasilimaliwatu na Utawala (DAHRAM), ambaye ndiye mratibu wa utekelezaji wa shughuli za mifumo ya serikali ndani ya Tume. 

Aidha Mndolwa aliwakumbusha wahandisi wa umwagiliaji wa Tume kwa mikoa kuwa wasimamizi wa shughuli za utekelezaji wa majukumu ya tume ndani ya mikoa yao. Aliongeza kuwa wahandisi hao watapimwa kwa utekelezaji wa majukumu hayo.

Katika kuhakikisha ufanisi, Bwana Mndolwa alisisitiza watumishi wote kuheshimu sheria za utumishi, ikiwemo kufika kazini kwa wakati na kuvaa mavazi yenye hadhi. Kuhusu mabadiliko ya uongozi, Bwana Mndolwa alisema ofisi yake inalazimika kufanya mabadiliko ndani ya idara na vitengo vya Tume ili kuongeza ufanisi.