Jumatatu , 10th Jun , 2024

Jeshi la Polisi kikosi cha kuzuia wizi wa mifugo kwa kushirikiana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi wamewakamata watuhumiwa wanne na ng’ombe 70 ambazo zilikuwa zinatoroshwa kwenda nchi jirani kinyume na utaratibu.

Baadhi ya Ng'ombe zilizokamatwa

Akitoa taarifa hiyo leo Juni 10,2024 wilayani Longido mkoani Arusha Kamanda wa Polisi Kikosi cha kuzuia wizi wa mifugo nchini Kamishna Msaidizi Mwandamizi wa Polisi SACP Simon Pasua, amesema kikosi hicho kinaendelea na operesheni yake nchi nzima ya kuwabaini baadhi ya watu wanaotorosha mifugo na kukwepa taratibu zilizopo.

SACP Pasua amesema watuhumiwa hao waliokamatwa wakisafirisha mifugo hiyo sabini majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za kiupelelezi huku akiweka wazi kuwa kikosi hicho tayari kina majina ya watu wanaojihusisha na utoroshaji wa mifugo ambapo amesema watuhumiwa hao pia watakamatwa wakati wowote.