Waziri wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi Mwigulu Lameck Nchemba ameivunja bodi ya shirikisho la vyama vya ushirika vya wakulima wa tumbaku mkoani iringa (ITICOJE) na kuwafukuza kazi viongozi wa vyama vya msingi vya ushirika vya wakulima hao wa tumbaku waliojaribu kujimilikisha matrekta yaliyokopwa na vyama vyao huku mkopo huo ukilipwa na wanachama.
Maamuzi hayo yamefikiwa katika kikao kilichoitishwa na waziri huyo kwakushirikiana na viongozi wa mkoa wa Iringa kwa lengo la kusikiliza malalamiko ya wakulima wa tumbaku mkoani iringa.
Wakulima hao wamewalalamikia viongozi wa shirikisho la vyama vyao (ITICOJE) kwa madai ya kuwanyonya na kuwalimbikizia madeni ambayo mengi hayawahusu na wala hawajashiriki katika maamuzi ya kuomba mikopo hiyo.
Malalamiko hayo ya wakulima karibu yamponze mkurugenzi wa benki ya CRDB tawi la Iringa waliotoa mkopo huo wenye dalili za ufisadi ambapo mkurugenzi wa tawi hilo Bibi Kisa Samuel alitakiwa kujibu kwanini benki hiyo imetoa mikopo hiyo yenye harufu ya ufisadi.
Baada ya mjadala wa masaa zaidi ya matatu na kusikiliza kero za wakulima waziri Mwigulu akabaini ufisadi unaofanywa na baadhi ya viongozi kwa kushirikiana na baadhi ya wanachama wasio waaminifu kujilimbikizia mali kwa migongo ya vyama wanavyovitumikia.