
Taarifa hiyo imetolewa na Mkurugenzi wa utafiti na matumizi na ya hali ya hewa nchini Bwana Ladislaus Chang'a, alipokuwa akiongea na East Africa Radio, na kusisitiza kuwa mvua hizo ni za msimu tu, na maeneo mengi ya nchi yanatarajia kupata mvua hizo.
"Kwa kifupi mvua zinazoendelea kunyesha ni mvua za msimu na si vinginevyo, isipokuwa tunachoweza kusema kama alivyozungumza Mkurugenzi Mkuu katika taarifa ya mwezi septemba ni kwamba kwa mwaka huu kunakuwa na tofauti kidogo kwamba mvua za msimu zinachagiza na kuwepo kwa mfumo wa hali ya hewa ya elnino", alisema Ladislaus Chang'a.
Bwana Chang'a amesema kutokana na hali hiyo maeneo mengi nchini yataendelea kupata mvua nyingi na kuwepo kwa matukio kwa baadhi ya maeneo, na kuwataka wananchi kufuatilia taarifa mbali mbali za hali ya hewa zinazotolewa.
"Maeneo mengi ya nchini kwetu yanatarajiwa kupata mvua nyingi na vile vile kuwa na matukio ya mvua kubwa kubwa katika baadhi ya maeneo, kwa hiyo ni vema tukaendelea kufuatilia taarifa mbali mbali zinazotolewa na mamlaka ya hali ya hewa ili kuweza kuchukua tahadhari na kuchukua hatua stahiki za kukabiliana na athari ambazo zinaweza kujitokeza kutokana na hali ya hewa ambayo inaweza kutokea", alisema Chang'a.
Pamoja na hayo Bwana Chang'a amewataka wakazi wa mabondeni kuchukua tahadhari, ili kuweza kujinusuru kwa hali yoyote ambayo inaweza kujitokeza.