Alhamisi , 11th Jan , 2018

Mtu mmoja mkazi wa kijiji cha Mwakisebe kata ya Kimaha wilayani chemba mkoani Dodoma amefariki dunia, huku watu wengine zaidi ya 2000 wakiwa hawana mahali pa kuishi baada ya nyumba zao kubomoka na nyingine kuzingirwa na maji, kufuatia mvua

zinazoendelea kunyesha wilayani humo.

Inadaiwa kwamba athari za mvua zimejitokeza katika vijiji vya Olboloti ,Kaloleni na Mrijo Chini ambavyo ndivyo vinavyodaiwa kuathiriwa zaidi na mafuriko hayo, na kwamba shughuli za uokozi zikiendelea .

Aidha Mwenyekiti wa kijiji cha Olboloti, Abdallah Suti amesema mvua iliyonyesha katika maeneo yao ni kubwa na kwamba haijawahi kutokea tangu miaka ya 1960

Kwa upande wake Mkuu wa Zimamoto na uokoaji kituo cha Dodoma Amiry Issa amesema kikosi kinaendelea na shughuli za uokozi kuzunguka vijiji hivyo huku akiwataka wananchi kutosogelea maeneo hatarishi.

Naye Mkuu wa wilaya ya Chemba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama Wilaya hiyo, Simon Odunga amesema kuwa eneo wanaloishi wananchi hao ni eneo hatarishi kwani wanazungukwa na milima huku akiwataka wananchi waliojenga katika maeneo ya mabondeni kuhama mara moja.