Jumatatu , 24th Mei , 2021

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Bi. Anna Henga amesema suala la mtoto wa kike kurudi shuleni mara baada ya ujauzito ni suala ambalo litamsaidia kumkomboa mtoto wa kike tofauti na watu wengine wanavyodhani kwamba litafanya matukio ya mimba shuleni kuongeze

Kulia ni Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) Bi. Anna Henga, Kushoto mwanafunzi akiwa ni mjamzito (picha kutoka mtandaoni).

Akizungumza katika mahojiano na kipindi cha Supa Breakfast, Bi. Henga amemshukuru Waziri wa Elimu kwa kuanza kufanyia kazi maboresho katika sera ya elimu hususan kipengele cha kumruhusu mtoto wa kike kurejea shuleni mara baada ya ujauzito kwani hili litasaidia kumkomboa mtoto wa kike.

“Suala la mtoto wa kike akipata ujauzito arudi shuleni, mijadala imekuwa mingi kwamba akirudi shule hatojifunza sio kweli kwani, tukiangalia nchi yenye hiyo sheria mimba hazijaongezeka, hii ni kumpa fursa ya pili mtoto wa kike ili arekibishe makosa yake,” amesema Henga.

Aidha, amesema kuwa licha ya sera ya elimu kuwa nzuri katika usawa wa jinsi katika elimu ya mafunzo bado zipo changamoto zinazokwamisha utekelezaji wake ikiwemo miundombinu kwa upande wa mtoto wa kike.

“Sera ya elimu ina vitu vizuri inaelezea usawa wa kijinsi katika elimu ya mafunzo, imetambua wanawake na wanaume changamoto zinzofanya isitekelezeke kirahisi katika shule, moja ni changamoto ya miundombinu ikiwemo vyoo shuleni hususan kwa watoto wa kike,” amesema Henga.